SAKATA LA VIJANA WALIOFUKUZWA JKT

 • Tarehe 17 Aprili 2021, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) General Venance Mabeyo alieleza katika hotuba yake kwa Rais Samia Suluhu kuwa wamewafuta kazi vijana 854 wa JKT baada ya vijana hawa kugoma kupangiwa eneo linguine la kazi na kushinikiza kuwa wapewe ajira kazini. Vijana hawa ni wale walioahidiwa ajira na Hayati Rais Magufuli na walikuwa wanajenga Ikulu ya Chamwino huko Dodoma. Video ipo kuthibitisha hili kwani Mwendazake alisema kuwa

  • Wasipangiwe kazi mahali popote pengine
  • Wakimaliza ujenzi waajiriwe jeshini

  Jenerali Mabeyo alisema kuwa walichofanya wale vijana ni sawa na uasi hata hivyo hawajashtakiwa na wamesafirishwa kurudi nyumbani kwa mujibu ya maelezo yake. Maneno haya yameibua maswali mengi kwani ni wazi kuwa vijana hawa hawakuzuka tu na hoja ya kuajiriwa jeshini bali ilikuwa ni ahadi iliyofanywa hadharani.

  Baada ya Fichua kuibua hoja nzito kuhusu ahadi walizopewa vijana hawa zinazoonekana wazi ni ahadi hewa, tumepokea taarifa zaidi kuhusu ufisadi, ulaghai na utumikishwaji wa vijana wa JKT. Tumekusanya ushahidi wa picha na nyaraka kuthibitisha matukio haya.

  Haya ni baadhi ya mambo tuliyobaini:

  1. Vijana wa JKT 556 walishiriki kwenye kujenga ukuta wa mgodi wa Mererani wa wakaitw JKT Operation Mererani . Hawa pia walishiriki kujenga maghorofa/nyumba za askari Magereza Ukonga na ujenzi ulikamilika 21/01/2020
  2. Wakati wa kuzindua nyumba hizi aliyekuwa Rais kipindi hicho Hayati Magufuli alisema “ WALIOSHIRIKI UJENZI WA NYUMBA ZA MAGEREZA NA WATAKAOENDELEA NA UJENZI NIMEWAAJIRI”
  3. Baada ya kumaliza ujenzi wa hizi nyumba za Magereza, Ukonga vijana hawa walipelekwa kwenye kikosi cha jeshi 831KJ  kusubiri kupangiwa majukumu mengine kwenye miradi ya ujenzi hii ifuatayo:
  • Nyerere Hydropower Project
  • Jingo la NEC- Dodoma
  • Bandari kavu – Kwala
  • Chuo cha Ualimu – Kasulu
  • Jengo la Aviation – Kijichi
  • SUA laboratory building
  • Mzumbe University Hostels
  • Makazi binafsi ya Magufuli Chato
  • Makazi binafsi ya mkuu wa JKT Major Gen Mbuge

  Uchunguzi wetu uligundua kuwa tarehe 30/12/2020 vijana 273 wakarudishwa majumbani kwao wakiambiwa wasubiri ahadi ya Rais ya kuwa wataajiriwa kwenye vyombo vya usalama hasa JWTZ.

  Kuna nyaraka zinaonyesha watu/vijana wa JKT 183 walikuwa wanasainishwa makaratasi kuwa wamelipwa 7,000/= TZS kila siku kwa siku 395 lakini hakuna hata mmoja aliyepewa hiyo hela. Chanzo chetu kimetueleza kuwa  jumla ya 505,995,000/= TZS(hizi zikiwa ni baadhi tu ya nyaraka chache tulizofanikiwa kuzipata)  walizokuwa walipwe hawa vijana vimeliwa na wakubwa huko JKT

  Kuna haja kubwa uchunguzi kufanywa ya kiina kuhusu utumikwishaji wa Vijana wa JKT katika miradi ya serikali na ahadi walizokuwa wanapewa za ajira. Tutaendelea kuweka ushahidi tutakazozikusanya

  Kama wewe pia ni muathirika wa sakata hili au una taarifa zaidi ya ufisadi uliofanywa kupitia JKT tuma maelezo na ushahidi kwenye channel yetu ya Signal namba +1 620 267 5770

  Hizi ni picha mbalimbali za majengo/miradi manayo vijana hawa wa JKT walihusika katika kuitekeleza kwa kujitolea kwa ahadi ya kuajiriwa jeshini lakini wameishia kuitwa waasi na kufukuzwa. Swali ambalo fichuaTanzania tunajiuliza ni kuwa toka lini waasi tena wakiwa na mafunzo ya kijeshi adhabu yao ni kurudishwa nyumbani?